Aliyekuwa msemaji wa klabu ya Yanga, Haji Manara, ametoa majibu makali kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, kufuatia kauli yake kuhusu uamuzi wa kuahirisha mchezo wa Kariakoo Derby uliopaswa kuchezwa Machi 8, 2025.
Katika majibu yake, Manara amemshutumu Karia kwa kile alichokiita “ulevi wa madaraka” na kusisitiza kuwa mechi hiyo haitachezwa hadi pale haki itakapotendeka. Aidha, amemtaka Rais huyo wa TFF kuomba radhi kwa kauli zake ambazo zimezua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau wa soka nchini.
Kauli ya Manara inakuja baada ya Karia kujibu tuhuma zinazoikumba Bodi ya Ligi kuhusu uamuzi wa kuahirisha mchezo huo maarufu. Karia, katika mahojiano na kituo kimoja cha redio, alisisitiza kuwa Bodi ya Ligi iachwe ifanye kazi yake na kwamba inafuata taratibu na sheria zinazopaswa kuzingatiwa.
Read Also: Haji Manara afungiwa na TFF | Haji Manara Banned For Two Years
“Taratibu tuziache zifuatwe, lakini huwezi kusema bodi ijiuzulu. Hata wanaosema hivyo wawaambie na viongozi wao, hawastahili kujiuzulu? Vitu vingine vinafanyika kitoto. Kama watu wamechoka kucheza mpira basi wakaendelee na sinema zao,” alisema Karia kwa msisitizo.
Hata hivyo, kauli hii haijampendeza Manara, ambaye alionekana kutofurahishwa na jinsi suala hilo linavyoshughulikiwa na uongozi wa TFF. Manara amedai kuwa bodi hiyo inapaswa kuwajibika kwa maamuzi yake, na siyo kutumia mamlaka kwa njia isiyo sahihi.
Mjadala kuhusu mchezo wa Kariakoo Derby umeendelea kuchukua nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, huku wadau wengi wa soka wakitoa maoni tofauti kuhusu mzozo huu. Mashabiki wa Simba na Yanga wanaendelea kufuatilia kwa karibu hatua zitakazochukuliwa na wahusika wakuu wa soka nchini Tanzania.
Kwa sasa, macho yote yameelekezwa kwa TFF na Bodi ya Ligi kuona iwapo suluhu itapatikana ili mchezo huo maarufu kuchezwa kama ilivyopangwa awali.
Leave a Comment