Vyakula vya kuimarisha misuli ya uume
TATIZO la kupungukiwa nguvu ni suala linaloumiza familia na kuvuruga mahusiano. Tatizo hili siyo tu linamuathiri mwanaume, lakini pia kwa kiasi kikubwa linamuathiri mkewe. Mwanamke ndiye anayejua kiwango cha nguvu za kiume za mumewe, yeye ndiye anayefahamu kuliko hata mwanaume mwenyewe. Vilevile wanawake wengi ndio huwa mstari wa mbele kumshauri na hata kumpeleka mumewe hospitali kutokana na tatizo hili. Wakati mwingine mwanaume anaweza kuona siyo tatizo labda ni hali ya mabadiliko ya kawaida, lakini kumbe ni tatizo.
JINSI HALI ILIVYO
Nguvu za kiume hutokea kutokana na uwepo wa msukumo mzuri wa damu katika misuli ya uume, misuli ya uume imeumbwa kama sponji ambapo msukumo wa damu unapoelekea kwa wingi na kwa nguvu sehemu hiyo misuli hushiba damu na kusababisha uume kuwa mzito na kusimama. Msukumo mkubwa wa damu katika misuli ya uume huchagizwa na kemikali ya Nitric oxide iliyopo katika kuta za mishipa ya damu ya misuli ya uume, vichocheo vya testosterone ambazo tunaziita homoni za kiume na virutubisho vinavyosababisha uimara wa nguvu za kiume ni vitamimi na madini mbalimbali.
Hali ya utulivu wa mwili hasa kisaikolojia husaidia akili iwe sawa na kuongeza na kukoleza uwezo wa kumudu tendo la ndoa. Mwili wenye nguvu pia utakuwezesha kulifanya tendo hili kwa ufanisi. Udhaifu wa mwili unaharibu uwezo wa kufanya tendo la ndoa, udhaifu unaotokana na maradhi mbalimbali kama kisukari, shinikizo la damu la juu, maumivu makali ya mwili, maambukizi sugu mfano kifua kikuu, HIV na maradhi mengine ya kuambukiza.
Matatizo ya kisaikolojia huweza kusababishwa na maradhi au maumivu ya mwili ya muda mrefu. Matatizo haya pia huchangiwa na hali ngumu ya maisha, migogoro na migongano ya kifamilia na kijamii na matatizo makubwa ya kifamilia mfano kuuguliwa, kufiwa na mengine. Mwili kuwa na nguvu au stamina husaidia katika suala zima la nguvu za kiume kwani husaidia kukoleza msukumo wa damu katika misuli ya uume na sehemu nyingine za mwili.
Mwanaume asiye na maradhi sungu au asiyetumia kilevi cha aina yoyote huwa anakuwa vizuri katika suala hili na
hali inakuwa nzuri zaidi kwa mwanaume anayefanya mazoezi, mazoezi aina yoyote iwe kukimbia au kucheza mpira ili mradi mwili unachemka na kutoa jasho.
AINA ZA VYAKULA VINAVYOONGEZA NGUVU ZA KIUME
Hivi ni vyakula vinavyotakiwa kuliwa kila siku au mara kwa mara, vyakula hivi ni vya asili na huwasaidia zaidi wale wasiokuwa na tatizo la nguvu za kiume. Kwa wale ambao tayari wana matatizo, basi ni vizuri waendelee kula vyakula hivi huku wakifanya uchunguzi na tiba hospitali. Ufanyaji wa mazoezi, pamoja na kufanya mazoezi tuliyoelezea mfano mazoezi ya kegel yawe ni sehemu ya maisha yako kwa kuwa hayahitaji uwanja mkubwa.
Vyakula vinavyoboresha nguvu za kiume kwanza ni vyakula vya wanga ambavyo kazi yake kubwa ni kutia nguvu mwilini, vyakula hivi ni kama ugali na wali, ulaji wake ni wa kawaida kutegemea na mahitaji ya mwili. Pia unywaji wa maji ya kutosha husaidia kupooza mwili na kusambaza virutubisho mwilini. Vyakula vyenye protini husaidia kujenga mwili na kurekebisha sehemu za mwili zilizochakaa au kuzeeka. Protini tunapata kwenye vyakula vyote vya jamii ya kunde, samaki, nyama na mayai. Pia vitamini ni muhimu sana, matumizi ya vitamini mwilini husaidia ufyonzaji wa baadhi ya madini, uyeyushaji wa mafuta na kusaidia vichocheo au homoni za kiume ziweze kufanya kazi pamoja na kemikali muhimu mfano Nitric Oxide.
Vitamini muhimu kwa nguvu za kiume ni kama vitamini A ambayo huhitajika mwilini kwa kiasi kukubwa nayo tunaipata kwenye mboga za majani lakini zaidi inayohitajika ni vitamini A ya omega three tunayoipata toka kwenye samaki ambayo husaidia kuamsha vichocheo vya Testosterone na kemikali ya Nitric Oxide kwenye uume hivyo kusaidia uume uwe na nguvu za kutosha. vitamini hii ya omega three tunaipata pia kwenye mafuta ya samaki. Samaki wenye kiwango kizuri cha vitamini A ya Omega Three ni jamii yote ya samaki wa baharini na zaidi ni pweza na jodari.
Aina nyingine ya vitamini muhimu kwa nguvu za kiume ni vitamini D ambayo pia tunaipata katika mafuta ya wanyama, samaki na pia vitamini hii huchagizwa na mionzi ya jua hasa jua la asubuhi, kazi ya vitamini hii ni kuamsha ufyonzwaji wa vichocheo vya Estrogen na madini ya calcium au chokaa mwilini pamoja na kuwa na kazi kubwa kwenye mifupa lakini vichocheo hivyo husaidiwa na vile vya kiume katika kuboresha hisia na hamu ya tendo la ndoa. Hali hii inapokuwa nzuri mwilini ndipo inamsaidia mwanaume anapata hali nzuri katika afya ya nguvu za uume iitwayo Morning Erection au urijali ambapo kila ukiamka asubuhi unakuta uume umesimama.
Vitamini C ni muhimu sana kwani ina kazi kubwa ya kuimarisha msukumo wa damu mwilini hasa katika usambazaji wa hewa ya Oksijeni kwenye tishu mbalimbali mwilini hasa kwenye misuli ya uume. Kazi hii hufanywa na chembechembe nyekundu za damu, hivyo Vitamini C husaidia ufyonzaji wa madini ya chuma toka kwenye vyakula tunavyokula kisha madini hayo husaidia kujenga seli hizo ambazo hubeba Oksijeni.
Vitamini C hupatikana kwenye matunda kama ndizi mbivu, machungwa, maembe, matikiti maji na jamii nyingine ya matunda kama haya.
Ulaji wake wa mara kwa mara husaidia sana kuboresha nguvu za kiume. Vitamini E, hii ni aina ya vitamini ambayo kazi yake kubwa ni kufungua tishu mbalimbali za ndani zaidi ili kuruhusu Oksijeni iingie, vichocheo na kemikali nazo ziingie na kutoka, kazi yake vitamini E ina uwezo wa kufanya kazi peke yake na huboresha misuli ya uume na mishipa ya damu. Vitamini hii pia huhitajika kwa kiasi kikubwa mwilini. Tunapata vitamini E toka katika mafuta ya mimea, karanga mbichi, nazi na kutoka katika baadhi ya mbegu mfano mbegu za maboga na jamii yake.
Madini pia ni muhimu kwa afya ya nguvu za kiume, madini huwa yanatoka ardhini, madini yanayohitajika mwilini ni mengi lakini yanayohitajika katika kuimarisha nguvu za kiume ni selenium, zink na potasium kwa kiasi kidogo. Madini ya potasium husaidia kuondoa uchovu wa mwili au fatique au hutamkwa fatiki, kutokana shuruba mbalimbali za kutwa nzima. Uchovu huu pia huchangia kupunguza kasi ya ufanyaji wa tendo la ndoa.
Mwanaume mwenye upungufu wa madini ya potasium mwilini huchoka sana baada ya kumaliza tendo la ndoa na huhisi mwili unauma. Madini hupatikana katika vyakula vya jamii ya mizizi na baadhi ya matunda kama tutakavyokuja kuona.