Bandari ya Dar kubinafsishwa, TPA yatoa ufafanuzi
Wakati mjadala kuhusu Azimio la Serikali ya Tanzania kuingia makubaliano na Serikali ya Dubai kwa ajili ya uendeshaji wa bandari ya Dar es Salaam ukipamba moto, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imekanusha baadhi ya mambo na kuwataka Watanzania kutosikiliza kile inachoita upotoshaji.
Ufafanuzi wa TPA umekuja ikiwa imepita siku moja tangu Kamati ya Bunge ya Miundombinu na uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ikipokea maoni ya wadau bungeni jijini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa na TPA jana Juni 6, imesema madai kuwa Serikali ina mpango wa kuipa kampuni ya DP World ya Falme ya Dubai kandarasi ya kuendesha bandari ya Dar es Salaam kwa miaka 100 siyo za kweli.
“Azimio la Bunge linalohusu mkataba ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaingia a Serikali ya Dubai wenye ukomo wa miezi 12 kwa ajili ya kutoa nafasi ambayo Serikali hizo mbili mbili zinaweza kushirikiana katika uboreshaji wa sekta ya bandari nchini Tanzania,” imesema taarifa hiyo.
TPA imefafanua kuwa ushirikiano wa nchi hizo mbili unalenga la kukuza ajira za Watanzania na kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kupitia uwekezaji kwenye baadhi ya maeneo ya bandari ya Dar es salaam, maeneo huru ya kiuchumi na viwanda na mnyororo wa usafirishaji kwenda nchi jirani.