LEARNING

Dua Za Ramadhani

Dua Za Ramadhani

Ramadhani ni mwezi mtukufu unaobeba baraka, rehema, na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Katika mwezi huu, Waislamu hukithirisha ibada na dua ili kujikurubisha kwa Mola wao. Dua ni silaha ya muumini, na katika mwezi huu mtukufu, kuna dua maalum zinazoweza kusomwa kila siku kutoka tarehe 1 hadi 30 ya Ramadhani.

Kila siku ya Ramadhani ina dua yake mahsusi, lakini pia zinaweza kusomwa mara nyingi kadri ya uwezo wa mtu. Hapa chini ni mpangilio mzuri wa dua hizi kwa ajili ya ibada yako.

Dua za Ramadhani kwa Kila Siku

  1. Ewe Mola! Nijaalie kufunga kwangu kiwe cha kweli na ibada zangu zikubalike. Uniepushe na uvivu na uzembe ili niweze kukamilisha ibada zangu kwa ukamilifu.
  2. Ewe Mola wangu! Nisongeze karibu na radhi zako, uniepushe na ghadhabu zako, na Unipe uwezo wa kusoma Qur’ani kwa wingi.
  3. Ewe Mola! Niruzuku utulivu na ufahamu, uniepushe na ujinga na uzembe, na unijaalie kupata fungu la baraka zinazoshuka katika mwezi huu mtukufu.
  4. Ewe Mwenyezi Mungu! Nipe nguvu ya kutekeleza amri zako, unijaalie utamu wa kukutaja, na unihifadhi katika ulinzi wako.
  5. Ewe Mola! Nijaalie kuwa miongoni mwa wanaotubu na wanaoomba msamaha, na unikaribishe miongoni mwa waja wako wema.
  6. Ewe Mwenyezi Mungu! Usiniruhusu kudhalilika kwa sababu ya makosa yangu, wala usiniruhusu nijiingize katika ghadhabu zako.
  7. Ewe Mola! Nisaidie kufanikisha funga yangu, nisimamie ibada yangu, na uniepushe na makosa.
  8. Ewe Mola! Niruzuku huruma kwa mayatima, kusaidia wenye shida, na kuwasalimia ndugu zangu Waislamu kwa amani.
  9. Ewe Mwenyezi Mungu! Nijaalie kupata fungu la rehema zako, uniongoze kwenye mwangaza wako, na unielekeze kwenye radhi zako.
  10. Ewe Mola! Nijaalie niwe mwenye kutegemea wewe pekee, na unijaalie kuwa miongoni mwa waja wako wema.
  11. Ewe Mola! Nipendezeshe kwa matendo mema na uniepushe na maovu na uasi.
  12. Ewe Mola! Nipambe na sitara ya kukuogopa na kunitosheleza kwa kila neema unazonipa.
  13. Ewe Mwenyezi Mungu! Nitakase na madhambi na unipe subira juu ya kila majaribu yanayonikumba.
  14. Ewe Mola! Nisamehe makosa yangu na uniongoze nisikumbwe na maangamizo.
  15. Ewe Mwenyezi Mungu! Niruzuku unyenyekevu na kunifungua moyo wangu kwa toba ya kweli.
  16. Ewe Mola! Niepushe na marafiki waovu na uniepushe na kila shari.
  17. Ewe Mola! Niongoze kutenda matendo mema na unitimizie haja zangu zote.
  18. Ewe Mwenyezi Mungu! Nijalie mwanga wa baraka za mwezi huu na unifanye niwe na moyo safi.
  19. Ewe Mola! Niongezee fungu la baraka za mwezi huu na unirahisishie njia ya kufanya wema.
  20. Ewe Mwenyezi Mungu! Fungua milango ya pepo na unifunge milango ya moto.
  21. Ewe Mola! Uniongoze kwenye njia sahihi na uniepushe na udanganyifu wa Shetani.
  22. Ewe Mwenyezi Mungu! Nifungulie milango ya fadhila zako na uniteremshie baraka zako.
  23. Ewe Mola! Nisafishe na madhambi na uniongoze kwenye uchamungu wa kweli.
  24. Ewe Mwenyezi Mungu! Nijalie kufanya mambo yanayokupendeza na uniondoe kwenye mambo yanayokuudhi.
  25. Ewe Mola! Nijalie niwapende watu wema na nifanye kuwa mwenye kushikamana na Sunna za Mtume Muhammad (S.A.W).
  26. Ewe Mola! Matendo yangu yawe yenye kupokelewa, madhambi yangu yasamehewe, na amali zangu zikubaliwe.
  27. Ewe Mwenyezi Mungu! Niruzuku neema zako na uniruzuku baraka na msamaha wako.
  28. Ewe Mola! Nijaalie unyenyekevu na kuzingatia nyakati za ibada.
  29. Ewe Mola! Nipunguzie mizigo ya madhambi na unijaalie rehema zako kwa wingi.
  30. Ewe Mwenyezi Mungu! Nijalie neema ya kuwa huru na moto wa Jahannam na unipe nafasi ya kuingia peponi.

Sikiliza: Qaswida Za Ramadhani: Kusherehekea Mwezi Mtukufu kwa Ibada Zenye Mtiririko wa Ladha

Ramadhani ni mwezi wa ibada na dua, na kila siku ina nafasi ya kipekee ya kupata msamaha wa Mwenyezi Mungu. Tunapaswa kutumia fursa hii kikamilifu kwa kusoma dua hizi, kufanya ibada kwa unyenyekevu, na kujikurubisha kwa Mola wetu. Mwenyezi Mungu atukubalie dua na ibada zetu katika mwezi huu mtukufu. Ameen!

Leave a Comment