LEARNING

Jinsi ya kuswali kwa Mwanamke wa Kiislam

Jinsi ya kuswali kwa Mwanamke wa Kiislam

Jinsi ya kuswali kwa Mwanamke wa Kiislam Amri hii ya Allah Subhanahu Wata’alah kama ilivyo ndani ya kitabu chake kitukufu kinawahusu waumini wote; mwanamume na mwanammke.

Sote tunakiri kuwa Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie ndiye mwalimu wetu mkuu.

Ni yeye ndiye aliyetufundisha swala na dini kwa jumla, lau kama si yeye tusingejua swala.

Ni yeye ndiye aliyetufundisha kwamba mwanamke anatofautiana na mwanamume katika baadhi ya mambo katika utekelezaji wa amri hio ya Allah ; amri ya swala.

Kwa mujibu mafundisho sahihi ya mtume, mwanamke anatofautiana na mwanamume katika mambo 5 yafuatayo ndani ya swala:-

1)  AJIKUSANYE MWILI WAKE KATIKA SIJIDA

Zoezi hili hutekelezwa kwa mwanamke kuvigusisha viwiko vyake vya mikono katika mbavu zake wakati wa kuitekeleza nguzo ya sijida. Kadhalika aliambatishe tumbo na mapaja yake.

Hivi ni kinyume atakiwavyo mwanamume katika kulitekeleza zoezi hili zima la kusujudu. Yeye hutakiwa avitenganishe viwiko na mbavu zake na alinyanyue tumbo lake lisigusane na mapaja yake.

Haya ndiyo mafundisho yanayotokana na riwaya:

“kwamba Mtume -rehma na amani zimshukie- aliwapitia wanawake wawili wakiwa wa naswali akawaambia:”mtakaposujudu zikusanyeni baadhi ya nyama mnapokwenda ardhini (kusujudu ), kwani mwanamke katika hilo si kama mwanamume.” Baihaqiy

2) ASHUSHE SAUTI YAKE MBELE ZA WANAMUME WA KANDO NA KANDO

Mwanamke anatakiwa aishushe sauti yake, asiitoe kiasi cha kusikika na wanaume wa kando na kando* wakati wanaposwali sala ambayo ni sunna kutoa sauti.

Hii ni kwa sababu ya kuchelea fitina inayoweza kuzuka nyuma ya pazia la sauti yake ambayo kwa mtazamo wa sheria kamaumbile ni pambo na kivutio tosha kwa mwanamume. Tusome na tuelewe:

“…. BASI MSILEGEZE SAUTI (zenu mnaposoma wa wanamume) ILI ASITAMANI MTU MWENYE UGONJWA MOYONI MWAKE ( kufanya mabaya na nyie) …”.(33:32)

Tumefahamu kutokana aya hii kwamba kuna uwezekano sauti ya mwanamke ikazusha fitna ambayo mwisho wake si mzuri.

Hii ndiyo falsafa ya Uislamu katika kuweka sheria ya hijabu hata katika eneo la sauti ya mwanamke akiachilia mbali mavazi na mchanganyiko wa mwanamume na mwanamke.

Kwa mantiki hii Uislamu unamtaka na kumuamrisha mwanamke muumini kuteremsha sauti yake mbele za wanamume hata akiwa ndani ya ibada ya swala. Hiyo ni ndani ya ibada seuze baki ya hali/ maeneo mengine!.

Hivi ni kinyume na mwanamume, yeye anatakiwa anyanyue na kutoa sauti mahala panapohitaji sauti kwa mujibu wa sheria.

3) APIGE KIKOFI AKIPATWA NA JAMBO NDANI YA SWALA.

Mwanamke atakapopatwa na jambo ndani ya swala na akataka kumtanabahisha mtu aliyeko pembeni yake jambo fulani.

Yeye anaelekezwa na sheria apige kikofi hafifu kama ishara ya kuashiriajambokwa aliye jirani.Namna ya kupiga ni kutumia tumbo la kitanga chake cha kulia kupiga juu ya mgngo wa kitanga cha mgongo wa kulia.

Wakati ambapo mwanamume anapopatwa na jambo/dharura nadani ya swala anatakiwa alete tasbihi kwa sauti yenye kusikika bila ya kuikusudia hiyo tasbihi.

Hivi ndivyo ilivyopokelewa kutoka kwa Sahli ibn Saad- Allah amwie radhi- kwamba Mtume -rehma na amani zimshukie-amesema,

“atakayepatwa na jambo (linalohitaji tanbiih) ndani ya swala na alete tasbihi, kwani atakapoleta tasbihi ataeleweka (na walio jirani naye). Na hakika si vinginevyo kupiga kofi ni kwa mwanamke” Bukhariy na Muslim.

4)  MWILI MZIMA WA MWANAMKE NI UTUPU(UCHI)

Kisheria mwli mzima wa mwanammke ndani ya swala na mbele ya mwanamume wa kando na kando ni utupu ila uso na viganja vyake.

Sehemu nyingine yote ya mwili wake ukiondoa uso na viganja ni wajibu ufunikwe na kusitiriwa kama tulivyo bainisha bayana katika darasa zilizotangulia ili linatokana na agizo lililoko katika kauli ya Allah subhana wataallah

“WALA WASIDHIHIRISHE VIUNGO VYA VYAO ISIPOKUWA VINAVYODHIHIRIKA (navyo ni uso na viganja vya mikono)” (24:31)

Imepokelewa hadithi kutoka kwa Ummu Salama Allah amuwie radhi-kwamba yeye alimuuliza Mtume rehma na amani zimshukie: je, mwanammke anaweza kusali akiwa amevaa kanzu (ndefu yenye kufunika mwli mzima) shungi tupu bila ya shuka ya chini? (mtume) akijibu:

“itakapokuwa kanzu hiyo ndefu yenye kufunika sehemu ya juu ya miguu yake” Abu Dawoud.

Ni dhahiri kuwa ikiwa kanzu hii itafunika kabisa sehemu ya juu ya miguu wakati wa kusimama na kurukuu, itajivuta wakati wa kusujudu na hivyo kufunika nyayo

Ama mwanamume ni ile sehemu iliyo baina ya kitovu na magoti.

Lau atasali akiwa amesitiri sehemu hiyo tu ya mwili wake na sehemu nyingine ikawa wazi, basi swala yake itasihi.

Hivi ndivyo inavyobainishwa na kauli ya Mtume kwa Allah rehma na amani zimshikie:

“sehemu iliyo juu ya magoti ni katika utupu na sehemu iliyo chini ya kitovu ni katika utupu”. Darulkutuniy na Baihaqiy

5) MWANAMKE HANA ADANA ANA IQAMAA TU.

Haikusuniwa adhana kwa mwanamke bali kilichosuniwa kwake ni iqama tu.Angalia lau mwanamke ataadhini kwa sauti ya chini si karaha na adhana yake hiyo itazingatiwa tu kuwa ni dhikri ambayo itampatia thawabu na haitazingatiwa kuwa ni mwito kwa swala.

ama akiinua sauti yake kiasi cha kusikika itakuwa ni karaha na ikichelea kuamsha fitna itakuwa ni haramu, elewa!

Hii ni tofauti na mwanamume, yeye amesuniwa kuleta adhana kwa kila swala ya fardhi hata kama anaswali peke yake.

Leave a Comment